Sunday, September 6, 2015

RAIS WANGU KIKWETE UONGOZI WETU KAMA KISHADA TUTOKAKO TUENDAKO HAKUJULIKANI!
Na Adelinus .D. Banenwa;.
Rais wangu moja kati ya sifa nyingi za mtu dhaifu ni uoga. Anaogopa hata kivuli chake. Serikali ya Awamu ya nne ikisikia kuna mgomo au hasa maandamano, inatetemeeeka, utadhani ni utete dhaifu unaosukumwa na mkondo mkali wa maji ya mto yaendayo kasi! Yohani, ‘John Pombe Magufuli’ ni uzao halisi wa udongo wa nchi hii. Amefukua vya kufukua!
Katumbua jibu na sasa usaha unamwagika. Mwenye jipu yaani serikali, inanuka usaha mwili mzima! Kwakuwa Wahenga wenye busara walisema dawa ya jipu ni kulitumbua na kwakuwa Waziri wetu wa Ujenzi amelitumbua, basi wote wenye mapenzi mema wanapaswa kumpongeza kwa kazi njema aliyoifanya.
Rais wangu palipo na ukweli tutasema. Lazima tuusimamie ukweli hata kama kwa kuusema ukweli huo mjinga atasema tunamchukia mtu na mpumbavu atasema tumenunuliwa na mtu! Kuacha kusema ukweli kwa kuogopa kuonekana unamchukia mtu au kuogopa kusemwa umenunuliwa ni upungufu alionao mwanadamu dhaifu. Jasiri hatikiswi na hilo!
Magufuli sifahamiani naye, lakini ni mtu mwema gani asiyeujua utendaji kazi wake ulivyo mahiri? Tangu waende akina Sokoine na Mrema nani mwingine wakutolea mfano?
Huyu siyo malaika. Aliposhirikiana na genge la walanguzi tukulangua nyumba zetu, wenyewe wakiziita za serikali tulimlaani wote! Na kwa hilo hajasamehewa! Na hatasamehewa mpaka pale atakapowarudishia wananchi nyumba zao! Lakini kwakuwa hatuko hapa kuangalia sura za watu, tuko hapa kujadili utendaji kazi mahiri kwa maslahi ya nchi yetu na wananchi wake, anayefanya jambo jema kama alilolifanya Magufuli, kusimamia sheria za nchi, hatuna budi tumpongeze wote.
Kiongozi wa haki mwenye ufahamu timamu akiambiwa ukweli hata kama utamuumiza, atamheshimu aliyemwambia huo ukweli, akijua kuwa huyo ndiye aliye na mapenzi ya kweli naye. Na ikimpendeza atamtumia!
Rais wangu wapinzani wanapokwambia waondoe mawaziri wanaokupotosha hawamchukii mtu wala hawawachukii hao mawaziri! Wanakutakia mema Rais wangu! Hawataki uonekane wa ajabu mbele ya watu wako! Tunaoishi na wananchi huku mitaani, vijijini na mashambani tunaambiwa mengi. Ningekuwa na faragha na wewe mengine ningekuwa nakunong’oneza, ili ukinieleza niwaeleze wapate kukuelewa kwa maana wako wanaokupenda! Kwa kuwa sina faragha na wewe nakuwekea maneno ya wananchi wako hapa ili ukiyasoma ujue ni picha gani wanaokuzunguka wanakutengenezea mbele ya wananchi!
Mwanamwema kutoka Iringa aliniandikia ujumbe ambao na mimi nauweka hapa vilevile alivyoandika! Aliandika, “Mwalimu nimesikitishwa sana na hotuba ya rais iliyoangaliwa hata na watoto wadogo. Hivi kwa nini anamshambulia mwananchi wake kwa maneno makali kama yale? Halafu kwa nini kila kitu anasema ‘nimeambiwa’? Falsafa yake ya mbayuwayu imemshinda? Sasa tena tunaambiwa kumbe hata mswada wenyewe hajausoma. Kazi tunayo. Nchi za kiafrika haziendelei na moja ya sababu ni kuongozwa na watu wenye kuambiwa.”
Rais wangu usipokuwa na pupa utaona kuwa watu wako wanakujali lakini unawakatisha tamaa! Dunia na Ulimwengu vinatambua hivyo! World Happiness Report 2013 iliyoandaliwa na kundi la wataalamu kutoka Umoja wa Mataifa imedai kuwa Watanzania ni miongoni mwa watu wasio na furaha na waliokata tamaa hapa Duniani!
Ndugu Rais yaliyojiri katika sakata la wenye malori na serikali limezidi kuwakatisha tamaa Watanzania. Iliandikwa, ‘Pinda amuonya Magufuli’, wengine wakaandika, ‘Serikali yamzima Magufuli’. Wananchi wakabaki kuulizana, hivi Pinda na Magufuli wako serikali mbili tofauti? Ni serikali gani hii yenye viongozi wenye kauli tofautitofauti? Hawakutani kwenye Baraza la mawaziri kuweka msimamo wa serikali?
Waliosema serikali inapasuka mwanzoni sikuwaelewa. Utoto siyo uchache wa miaka ya kuzaliwa peke yake! Wala kufanya upuuzi siyo lazima umtukane mtu. Kwakuwa hawa ni waheshimiwa huwezi kuweka neno watoto au wapuuzi. Isipokuwa viongozi wa serikali moja kuonekana mbele ya wananchi kama wanatunishiana misuli, ni vyote viwili, utoto na upuuzi!
Rais wangu Magufuli anasema anazilinda barabara zetu zisife haraka! Mpaka hapa kuna ubaya gani? Je, mamlaka hayo anayo? Kaonyesha sheria iliyotungwa na Bunge kihalali kabisa! Kumbe mamlaka anayo kufuatana na sheria! Sasa ndugu Rais huyu anayemzima Magufuli au kumuonya yeye alisomea wapi?
Kwa mdomo wake Waziri Mkuu wetu anasema, “Hatua zilizochukuliwa na Dk Magufuli kufuta vifungu vilivyokuwa vikiruhusu asilimia tano zilifuata sheria. Tatizo lililojitokeza ni kutoshirikisha pande zinazohusika ili kushauriana na kupata uamzi wa pamoja”. Jamani sheria ikishatungwa mnashauriana nini tena?
Akaongeza, “Sasa suala la asilimia tano, lilitokana na ombi la wadau wa usafirishaji kwa aliyekuwa waziri wa Ujenzi miaka ya nyuma na haikuwa sheria kamili. Limeondolewa baada ya kuonekana linatumiwa vibaya.” Kudai kwa nguvu wakati huna sheria nikufanya fujo!
Bado anakiri kuwa limeondolewa baada ya kuonekana linatumiwa vibaya! Yaani wenye malori walitumia vibaya ombi lao. Magufuli kuona hivyo amelifuta. Kwa maelezo haya ya Waziri mkuu Magufuli amekosea wapi? Kama ombi hilo ovu liliridhiwa na Waziri wa Ujenzi wa miaka ya nyuma kwa maslahi ya nchi au kwa maslahi ya wenye malori na waziri mwenyewe haijulikani. Kinachojulikana ni kwamba waziri huyo hivi sasa serikali imemfikisha mahakamani kwa tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka alipokuwa ofisini siku hizohizo za nyuma.
Waziri mkuu anasema kosa la Magufuli ni kuilinda hiyo sheria bila kuwashirikisha wanaoivunja. Jamani, unapomkamata mwizi unamshirikishaje? Unashauriana naye nini ili mpate uamuzi wa pamoja kama siyo kutaka kumwomba rushwa?
Mzee Peter Kisumo anasema, “Chama kimebaki cha walalamikaji, kila mtu amekuwa mlalamikaji. Hata Waziri mkuu amegeuka mlalamikaji. Sijaona watu wanaowajibishwa kwa ufisadi!”
Rais wangu bado Waziri mkuu bila sababu ya msingi anaunda tume sijui kamati ambayo hata hivyo haina uwezo wa kuifuta wala kuirekebisha sheria hiyo! Huku ni kufuja kodi ya wananchi? Ndugu Rais ni hivi majuzi tu wananchi kwa huzuni kubwa wameshuhudia mwandishi wa habari Ufoo Saro, baada ya kujeruhiwa vibaya kwa risasi kadhaa wanawema walimkimbiza hadi Hospitali ya Serikali ya Tumbi lakini akakosa huduma ya matibabu kwasababu Hospitali hiyo haikuwa na mashine ya Xray.  Kwanini fedha zitakazotumika na tume hii na tume nyingine za aina hii zisingetumika kununulia mashine ya Xray kwa Hospitali hii? Umuhimu wa Hospitali ya tumbi uko wazi. Inapokea majeruhi kila siku watokanao na ajali za mara kwa mara zitokeazo katika barabara hii katili ya Morogoro! Mungu huyu! Maisha ya wananchi hayana maana mbele ya wenye malori!
 Serikali inayojiendesha bila kutegemea ufadhili wa wafanyabiashara hasa wakati wa kampeni, wenye malori wangepata wapi kiburi cha kugoma? Sheria kama haifai hurudishwa Bungeni ikafutwe au ikarekebishwe huku kazi zikiendelea! Wakati wa Uwaziri mkuu wa Sokoine au wakati wa Mrema, mwenye lori gani angethubutu kuinua pua yake juu? Serikali kuruhusu kikundi fulani cha watu, wawe wenye malori au wenye asili fulani, waendelee kuvunja sheria halali huku wananchi wengine wakiona ni mfano halisi wa uongozi mbovu! Bila kufahamu serikali inawasukuma na wengine wavunje sheria zinazowakera. Chanzo cha maandamano na migomo isiyokwisha ni uongozi mbovu!
Ndugu wananchi kitabu cha mwalimu mkuu wa watu kinaelekeza wazi kuwa jiandaeni kupokea fedha zitakazochangwa na hawa jamaa. Mkiletewa wakati wa kampeni zichueni, lakini kura msiwape! Kuita wenye malori ili muafikiane wakati sheria iko wazi ni kielelezo cha uongozi ulioshindwa kuongoza! Yanini Kuwa na kiongozi wa namna hiyo? Tumeliona hili kwenye tozo ya simu. Baada ya kusikia kelele za wananchi ikaamriwa mawaziri na wamiliki wa kampuni za simu au wadau wakae pamoja wafikie muafaka. Kiko wapi! Uongozi ulioshindwa!
Rais wangu uongozi wa nchi unapokuwa laini kiasi hiki, wananchi wanapoletewa habari za kutisha kuwa magaidi wameshamiri nchini mwetu matumaini yao wayaelekeze wapi? Jeshi la Polisi mkoani Mtwara, linawashikilia vijana 11 kwa tuhuma za kukutwa mafichoni katika msitu wa mlima Makolionga wilayani Nanyumbu wakifanya mazoezi ya kijeshi. CD walizokutwa nazo ni za kundi la kigaidi la Al Shabaab. Zinaonyesha watu wakichinjwa, mauaji ya kiongozi wa Al Qaeda Osama Bin Laden, Zindukeni Zanzibar, kuaandaa majeshi, mauaji ya Idd Amin na Mogadishu Sniper.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mtwara Zellote Stephen anasema watuhumiwa walikamatwa, baada ya polisi kupata taarifa kutoka kwa wasamaria wema. Wananchi wanauliza bila wasamaria wema magaidi hao si wangemaliza mafunzo yao halafu wakaenda kwenye utekelezaji bila polisi kuwa na habari? Polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama vilikuwa wapi?
Katikati ya habari hizo zinakuja habari nyingine zinazoarifu kuwa, Ramadhani Twaha mkazi wa mtaa wa Kirumba jijini Mwanza amefikishwa katika mahakama ya Mkoa wa Mara. Anatuhumiwa kukutwa akisambaza CD zenye machapisho ya kigaidi katika msikiti wa Ibadhi ulioko mjini Bunda ambazo zina mafunzo ya kijeshi na zinazochochea vurugu. Matukio haya mawili yanaashiria jinsi mtandao wa kigaidi ulivyosambaa nchini. Zinaingizwa vipi na kusambazwa vipi nchini? Nani wanaingiza CD hizi? Usalama wetu ni wa mashaka matupu!
Mafunzo  katika msitu wa Makalionga yalifanywa kwa muda gani? Je, kundi hilo la watu 11 lilikuwa ni kundi la ngapi? Ni katika msitu wa Makalionga tu ndiyo mafunzo hayo yanakofanyika? Je, waliyokuwa wanapewa mafunzo waliambiwa malengo ya mafunzo hayo? Walimu wao wako wangapi na wako wapi? Wanafadhiliwa na nani? Je, huu siyo mwanzo wa vita vya msituni?
Ndugu Rais raia kutoa taarifa kama hiyo kwa jeshi la polisi ni muhimu na ni ishara ya uzalendo kwa nchi yake, lakini huko kuwe ni kusaidia tu! Hilo ni jukumu la polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kugundua vyenyewe hatari zinazolinyemelea Taifa letu! Liwalo na liwe, wenye malori tu hivi! Magaidi mtawaweza vipi?
Rais wangu tunaacha ya kwetu tunadandia ya wengine. Viongozi wako kimbelembele kusaka sifa za bei poa. Nchi yetu ilipopata nafasi adhimu ya kulihutubia Baraza la Umoja wa Mataifa baadhi ya wananchi walisikika wakiusikitikia muda ambao kwa maoni yao uliotumika vibaya kuisema ICC badala ya kuyapa nafasi matatizo lukuki yanayoisibu nchi yetu! Nchi yetu ina ugomvi gani na ICC?
Rais wangu ni uzalendo kwa bara la Afrika na Waafrika wenzetu ndiyo vinatusumbua? Hapana! Ni mihemko ya moyo kwa kujihisi tuko kwenye foleni ya kwenda huko kutokana na tunayoyatenda nchini mwetu? Hili linawezekana! Kwanza ziliisha sikika habari kuwa kuna baadhi ya matukio ya kinyama yaliyotokea nchi mwetu ambayo taarifa zake zinatumwa huko! Kujitoa ICC hakuwezi kuzuia tusihukumiwe na mahakama nyingine. Kinachoweza kuzuia tusihukumiwe ni kutotenda unyama dhidi ya raia wetu, kama tunaona tunatenda.
Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa Bwana Koffie Annan amesema ‘itakuwa ni alama ya aibu’ kwa bara la Afrika iwapo litajiondoa katika mkataba wa Roma uliounda Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC. Amesema ikiwa viongozi wa Afrika wataipinga na kuipiga vita ICC na kujiondoa, itakuwa ni fedheha kubwa kwa kila mmoja wao na nchi zao. Tumwombee kwa Mungu Rais wangu asije akawa mmoja wao kati ya marais wanaotaka kuziletea nchi zao fedheha hii kubwa! Mwenye fikra ya kulipeleka wazo hili Bungeni huyo ni mufilisi, hafai kuwa kiongozi wetu! Tuna akili gani kubwa ya kutaka kuunga mkono kujitoa ICC kuliko akili ya viongozi waliotutangulia, waliosaini mkataba wa Roma wa kujiunga na ICC?
Bwana Annan amewashutumu viongozi wa Afrika kwa kulinda maslahi yao binafsi na si kwa Waafrika wote huku akisisitiza kuwa njama za nchi za Afrika kutaka kujiondoa ICC ni ishara dhahiri kuwa kuna desturi ya kutoheshimu sheria.
Watuhumiwa wanaokabiliwa na mashtaka katika mahakama hiyo wamefikishwa kama watu binafsi na si kama Bara la Afrika, hivyo dhana kuwa ICC ina dhamira ya kuwaandama viongozi wa Kiafrika siyo sahihi!
Mtu mzima tena bila aibu anasema kati ya walioshitakiwa 30 waafrika ni 27. Hawa ndiyo wale ambao akishtakiwa mhalifu, kama dini yao ni moja anasema wa dini yetu tunaonewa! Kiongozi kuishiwa fikra ni hatari sana. Muhimu hapa ni kujua je, walioshtakiwa ni wahalifu? Muhimu siyo rangi ya ngozi yao.
Mwanamwema Jaji mpya wa Mahakama ya kimataifa ya Uhalifu (ICC) Dk Steven Bwana amesema viongozi wa nchi za Afrika wanaotaka kujiondoa kwenye mahakama hiyo, wana lengo la kuficha uovu uliopo katika nchi zao kwani baadhi yao wanajifanya miungu watu!
Amesema, “Afrika kuna viongozi wazuri, lakini tusifiche ukweli wapo waovu, wengine nusu miungu wanaopenda kila kitu kiwe chao, hili halikubaliki. Nchi za kiafrika kujitoa ni aibu, sababu zilizotufanya tujiunge zipo, tunataka kujiondoa kwasababu tunadhani ICC inatufuatilia tunapofanya makosa, ICC inatimiza wajibu, haiwadhalilishi viongozi wa Afrika, watafika kote.”

No comments:

Post a Comment