Hivi ndivyo helikopta ilivyomuua shujaa Filikunjombe
Chopa (helikopta) aliyokuwa akitumia Mbunge wa jimbo la ludewa, Mhe. Deo Filikunjombe.
AJALI ya chopa (helikopta) iliyotokea
usiku wa kuamkia jana, Oktoba 16, 2015 katika Hifadhi ya Selous, eneo la
Msolwa mkoani Morogoro, imeyakatisha maisha ya aliyekuwa Mbunge wa
jimbo la ludewa, Mhe. Deo Filikunjombe (43), pamoja na watu wengine
watatu waliokuwa ndani ya helikopta hiyo,
Deo Filikunjombe.
Kwa mujibu wa taarifa zilizothibitishwa
na Kamishna wa Oparesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Paul Chagonja,
Mhe. Filikunjombe aliyekuwa akitetea ubunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya
Chama Cha Mapinduzi (CCM), alikuwa na watu wengine watatu kwenye
helikopta hiyo, akiwemo rubani, Kepteni William Silaa ambaye ni baba wa
Jerry Silaa, Vitalis Blanka Haule anayetajwa kuwa ndugu wa Filikunjombe
na Egdi Mkwera, Ofisa Tawala wa Mkoa wa Tarime na mtaalam wa mifugo.
Polisi na wananchi wakiwa eneo la tukio baada ya Chopa kuteketea kwa moto.
Chagonja alieleza kuwa helikopta hiyo
yenye namba za usajili, 5Y-DKK ilikuwa ikitokea jijini Dar es Salaam
kuelekea kusini huku taarifa nyingine zikieleza kuwa ilikuwa ikielekea
jimboni kwake, Ludewa kabla ya kupata hitilafu ya injini ikiwa angani,
baadaye ikaanguka na kulipuka, ikisababisha eneo lote la ajali kugubikwa
na vumbi na moshi mzito.
Habari zisizo rasmi zilizolifikia gazeti
hili, zilieleza kuwa helikopta hiyo iliondoka jijini Dar es Salaam
majira ya saa 9 alasiri. Kabla ya kuruka angani, vyanzo vyetu vinaeleza
kuwa helikopta hiyo ilipata hitilafu ndogo za kiufundi ambazo hata hivyo
zilirekebishwa na safari ikaanza bila matatizo.
“Ilipofika kwenye Hifadhi ya Selous,
rubani aligundua kwamba kuna hitilafu kwenye injini, akawa anajaribu
kutafuta sehemu ya kutua kwa dharura ndani ya hifadhi hiyo lakini kabla
hilo halijatimia, helikopta ilipoteza mwelekeo kabla ya kudondoka na
hatimaye kulipuka,” kilieleza chanzo chetu kwa sharti la kutotajwa jina
gazetini.
…Wakiendelea kufanya uchunguzi eneo la tukio.
Habari nyingine zinazosambaa kwenye
mitandao ya kijamii, zinaeleza kuwa helikopta hiyo ilianza kuwaka moto
ikiwa angani kabla ya kuanguka kandokando ya Mto Ruaha unaopita ndani ya
hifadhi hiyo ambapo baadhi ya maoni yalidai huwenda chopa hiyo
ilihujumiwa na hivyo kutaka uchunguzi zaidi.
No comments:
Post a Comment