Kafando arejea rasmi madarakani Burkina Faso
Rais Michel Kafando wa Burkina Faso aliyekuwa amepinduliwa kwa wiki moja
amerejea rasmi madarakani huku Umoja wa Ulaya ukisema ni hatua muhimu
ya kulirejesha taifa hilo kwenye utawala kamili wa kiraia.
Huku mitaa ya mji mkuu, Ougadougou, ikitandwa na nderemo na vifijo na
vijana wakiimba wimbo wa taifa, Rais Michel Kafando alirejea rasmi
kwenye ikulu jioni ya jana, wiki moja kamili baada ya jenerali mmoja wa
kijeshi na wafuasi wake kumuondoa madarakani na serikali yake ya mpito.Hata hivyo, sherehe rasmi za kurejea madarakani kwa Kafando na Waziri Mkuu Yacoub Isaac Zida zilifanyika bila kuhudhuriwa na kiongozi wa jaribio la mapinduzi yaliyoshindwa, Jenerali Gilbert Diendere, ambaye alilazimika kusaini makubaliano ya kuachia madaraka baada ya jeshi tiifu kwa serikali kumpa muda wa masaa 48 kufanya hivyo, ama vyenginevyo kukabiliwa na hatua kali.
Katika hotuba yake kwa taifa, Rais Kafando aliwashukuru wananchi na jumuiya ya kimataifa kwa kumuunga mkono muda wote. "Kusingekuwa na namna nyengine zaidi ya hii kufuatia kilio cha umma dhidi ya watenda uovu na lawama za kimataifa dhidi ya waliojichukulia madaraka kwa nguvu, na japokuwa serikali yangu ya mpito yenyewe haikuwa imechaguliwa kwenye uchaguzi huru, muliiamini na bado ndicho chombo pekee kinachowakilisha matakwa ya umma wa taifa hili," alisema Kafando.
Muda mchache baada ya Rais Kafando kuhutubia taifa, kiongozi wa mapinduzi hayo yaliyoshindwa, Jenerali Diendere aliliambia shirika la habari la AFP kwamba kitendo chao kilikuwa kosa lililokosa uungwaji mkono wa umma.
"Mapinduzi yamekwisha. Kufanya mapinduzi haya lilikuwa kosa kubwa kuliko yote. Tumejuwa kuwa umma haukuyataka. Na ndio maana tumeondoka," alisema mkuu huyo wa zamani wa ujasusi kwenye serikali ya Rais Blaise Compaore.
Rais Compaore mwenyewe alilazimika kuikimbia nchi mwezi Oktoba mwaka jana, baada ya kukabiliwa na maandamano ya umma.
Ushindi wa ECOWAS
Kushindwa kwa mapinduzi hayo na kurejea madarakani kwa Rais Kafando kunatokana kwa kiasi kikubwa na juhudi za Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS), ambayo ilianzisha haraka mchakato wa kurejesha utawala wa kiraia mara tu baada ya mapinduzi kutangazwa.
Umoja wa Ulaya, ambao ulikuwa umeungana na jumuiya ya kimataifa kuyalaani mapinduzi hayo, umeikaribisha hatua ya kurejea madarakani kwa Kafando. Taarifa iliyotolewa na Umoja huo kutokea Brussels, inasema kurejea kwa Kafando kunasawazisha hali ya mambo nchini Burkina Faso, wakati taifa hilo likielekea kwenye utawala kamili wa kiraia.
Kabla ya mapinduzi hayo, uchaguzi mkuu ulikuwa umepangwa kufanyika tarehe 11 Oktoba, lakini sasa Waziri Mkuu Isaac Zida amesema uchaguzi huo umesogezwa mbele kwa wiki kadhaa kutokana na sababu za kiufundi.
No comments:
Post a Comment